ZIKIWA zimebaki siku moja kabla ya kufunguliwa kwa dirisha dogo la
usajili hapa nchini, uongozi wa Yanga unajipanga vilivyo kuhakikisha
unakiimarisha kikosi chake ili kiweze kufanya vizuri katika mechi zake
zijazo za Ligi Kuu Bara lakini pia katika michuano ya kimataifa
Uongozi unahitaji kusajili wachezaji wanne katika dirisha hili dogo la
usajili kwa ajili ya kuziba upungufu uliojitokeza katika kikosi hicho
tangu kuanza kwa Ligi Kuu Bara msimu huu katika nafasi ya ulinzi, kiungo
pamoja na ushambuliaji. Na tayari mazungumzo na straika mmoja wa Kagera
Sugar yanaendelea.
Hata hivyo, habari za kuaminika kutoka ndani ya Yanga ambazo Championi
Jumatatu limezipata zimedai kuwa mpaka sasa uongozi huo umeishaanza
mazungumzo
na baadhi ya wachezaji ambao inawahitaji akiwemo Mtogo Vincent Bossou
ambaye ilimuacha baada ya kumalizika kwa msimu uliopita lakini pia
kiungo wa Mtibwa Sugar, Mohamed Issa ‘Banka’.
Ukiachana na wachezaji hao ambao taarifa zao zimekuwa zikisemwa sana
hivi karibuni pia uongozi huo unadaiwa kuwa katika mazungumzo na Straika
wa Kagera Sugar, Jafar Kibaya ambaye ni kati ya washambuliaji mahiri
hapa nchini.
Mshambuliaji huyo ndiye aliyeivuruga ngome ya Yanga kwenye mchezo wa
Ligi Kuu Tanzania Bara msimu huu alipoifungia timu yake bao moja wakati
Yanga iliposhinda 2-1 na kuwazidi ujanja mabeki wawili matata wa timu
hiyo, Kelvin Yondani na Andrew Vicent Dante ambao imekuwa adimu sana wao
kufungwa msimu huu.
Akizungumza na Championi Jumatatu, mmoja wa viongozi wa Yanga ambaye
aliomba kutotajwa jina lake, alisema uongozi huo unajipanga kuhakikisha
unamsajili Kibaya ili kuiongezea nguvu safu yake ya ushambuliaji ambayo
tangu kuanza kwa ligi kuu imekuwa ikiwategemea Ibrahim Ajibu pamoja na
Mzambia, Obrey Chirwa.
“Kwa hiyo kutokana na hali hiyo tumeona ni bora tupambane kuhakikisha
tunamsajili Kibaya kwa ajili ya kuja kusaidiana na wachezaji hao kwani
Donald Ngoma na Amissi Tambwe kwa sasa siyo wachezaji wa kuwategemea
sana.
“Muda mwingi wamekuwa nje ya uwanja, jambo ambalo linatufanya tuwe na
wakati mgumu pindi wanapoumia, kwa hiyo Kibaya anatufaa na tayari kocha
ametuambia tuhakikishe tunamsajili kwani alimuona tulipocheza na Kagera
Sugar kwenye Uwanja wa Kaitaba na alitusumbua sana,” alisema kiongozi
huyo.
Katika mchezo huo dhidi ya Yanga, Kibaya ndiye aliyefunga bao pekee la Kagera ambapo Yanga ilishinda 1-2.
Alipoulizwa suala hilo, Katibu Mkuu wa Yanga, Charles Mkwasa alisema:
“Muda wa usajili bado haujafika kwa hiyo kwa sasa siwezi kuzungumzia
hilo, tusubiri kwanza mpaka utakapofika muda huo.”
Hata hivyo, Meneja wa Kagera Sugar, Mohamed Hussein alipoulizwa kama
wapo tayari kumuachia mchezaji huyo ajiunge na Yanga alisema: “Waje
tuzungumze kama watakuwa tayari kutupatia fedha ambayo tutawaambia haina
shida kwani Kibaya bado ana mkataba wa miaka miwili na sisi.
“Tumemsajili msimu huu akitokea Mtibwa Sugar kwa hiyo wakikubali kutupatia fedha tutakayowaambia basi tutawapatia.”