Unaweza kujiuliza ni kwa jinsi gani ukatae kuwauzia wateja ambao wanataka kununua kwako wakati lengo lako kwenye biashara ni kuongeza wateja.
Lakini huo ndio ukweli, kuna wateja wengi ambao wanataka kununua kwako lakini wewe hutaki kuwauzia. Wateja wapo tayari kukupa fedha uwape huduma au bidhaa unazotoa lakini wewe hutaki kupokea fedha hizo. Unaweza kuwa unafanya hivyo kwa kujua au kwa kutokujua.
Leo kupitia mtandao huu wa NAPENDA BIASHARA, utajifunza kuhusu wateja hawa na kama utachukua hatua mara moja utaweza kuikuza biashara yako kwa kuwafikia wateja wengi zaidi.
Karibu ujifunze kuhusu wateja hawa ambao umewapa mgongo na hivyo kukosa fursa ya kukuza biashara yako zaidi.
Wateja uliokuwa unafanya nao biashara ila sasa huwaoni tena.
Kama umekuwepo kwenye biashara kwa muda sasa, kuna wateja wengi ambao ulikuwa unafanya nao biashara, ila sasa hivi huwaoni tena. Kama wewe umechukulia ni hali ya kawaida tu kwa wateja kuondoka, basi jua umeamua kuacha kuwauzia wateja waliokuwa tayari kununua kutoka kwako.
Watafute wateja hawa, jua wako wapi na kwa nini kwa sasa huwaoni kwenye biashara yako. Unaweza kuwafikia kwa kuwatumia ujumbe juu ya bidhaa au huduma mpya inayopatikana kwenye biashara yako kwa sasa.
Usiache wateja wapotee kwenye biashara yako, kama kuna mabadiliko uliyofanya na yakawafanya wateja waondoke kwenye biashara yako, basi yajue na jua ni hatua gani unaweza kuchukua.
Wateja ambao hawana uhakika.
Kuna wateja ambao wangependa kununua kutoka kwako ila hawana uhakika au imani kama wakinunua watanufaika kweli. Labda wana wasiwasi ubora unaweza usiwe mzuri. Labda wana wasiwasi kama kile wanachonunua hakitatimiza mahitaji yao basi watakuwa wamepoteza fedha zao.
Wajue wateja hawa kwa jinsi wanavyotoa sababu zao za kutokununua na wape uhakika. Unaweza kuwapa uhakika kwamba kama wanachonunua hakitawasaidia au wanaweza kurudisha na kurudishiwa fedha walizolipa.
Kulingana na biashara yako ilivyo, tafuta njia ya kumpa uhakika mteja ili aweze kufanya maamuzi ya kununua
.
Watu wa karibu kwa wateja wako.
Kama kuna wateja ambao wanaridhika na bidhaa au huduma unazowapatia, basi kuna watu wa karibu kwao ambao nao wangeweza kunufaika kama wao wanavyonufaika. Hawa ni wateja ambao umeamua kutokuwauzia ila wapo tayari sana kununua kutoka kwako.
Cha kufanya hapa ni kuwashawishi wateja wako wa sasa ambao wanaridhika na huduma zako kuwashirikisha watu wao wa karibu ili nao waje kununua kwako. Watu wa karibu wanaaminiana sana na kama mtu atamwambia mtu anayemjua kuhusu biashara yako, na akawa na shida kweli ni lazima atakuja kununua kwako.
Anza kuwapa msisitizo wateja hawa ambao wapo tayari kununua kutoka kwako ila wewe umewapa mgongo. Hawa ni wateja wazuri sana ambao huhitaji kutumia nguvu nyingi kuwapata.
Mbinu yoyote ya kuongeza wateja unayopanga sasa, hakikisha inaanza na wateja hao wa aina tatu. Hao wapo tayari kuliko wengine wengi utakaokuwa unawakimbilia.
Kwa ushauri na mwongozo zaidi wa biashara yako piga simu 0713 666 445
JIFUNZE BIASHARA, PENDA BIASHARA.
Ukijenga utamaduni wa kutembelea mtandao huu kila siku muda si mrefu unakuwa tajiri wa mali, maarifa na afya. Kazi kwako!
Download Video and Put Comment
Toa Maoni Hapa Chini
0 comments:
POST A COMMENT